Isaiah 35

Furaha Ya Waliokombolewa

1 aJangwa na nchi kame vitafurahi;
nyika itashangilia na kuchanua maua.
Kama waridi,
2 blitachanua maua,
litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha.
Litapewa utukufu wa Lebanoni,
fahari ya Karmeli na Sharoni;
wataona utukufu wa Bwana,
fahari ya Mungu wetu.

3 cItieni nguvu mikono iliyo dhaifu,
yafanyeni imara magoti yaliyolegea,
4 dwaambieni wale wenye mioyo ya hofu,
“Kuweni hodari, msiogope;
tazama, Mungu wenu atakuja,
pamoja na malipo ya Mungu,
atakuja na kuwaokoa ninyi.”

5 eNdipo macho ya vipofu yatafumbuliwa
na masikio ya viziwi yatazibuliwa.
6 fNdipo kilema atarukaruka kama kulungu,
nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe.
Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika,
na vijito katika jangwa.
7 gMchanga wa moto utakuwa bwawa la maji,
ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi.
Maskani ya mbweha walikolala hapo awali
patamea majani, matete na mafunjo.

8 hNako kutakuwa na njia kuu,
nayo itaitwa Njia ya Utakatifu.
Wasio safi hawatapita juu yake;
itakuwa ya wale watembeao katika Njia ile;
yeye asafiriye juu yake,
ajapokuwa mjinga, hatapotea.
9 iHuko hakutakuwepo na simba,
wala mnyama mkali hatapita njia hiyo,
wala hawatapatikana humo.
Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko,
10 jwaliokombolewa na Bwana watarudi.
Wataingia Sayuni wakiimba;
furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao.
Watapata furaha na shangwe;
huzuni na majonzi vitakimbia.
Copyright information for SwhNEN